Wednesday, October 3, 2012

MSANII DIAMOND ASAINI MKATABA NA KAMPUNI


Msanii Diamond Platnumz (wa pili kulia) akibadilishana mkataba wa kusimamiwa na mkurugenzi wa kampuni ya I-View Studios, Raqey Mohammed (kushoto) baada ya kusaini. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni mwanasheria wa Diamond, Paul Mgaya, mwanasheria wa I-View Dr. Peter Aringo na mkurugenzi wa One Touch Solutions, Petter Mwendapole.

MSANII wa kimataifa wa Tanzania, Naseeb Abdul a.k.a Diamond Platnumz ameingia mkataba na kampuni ya I-View Studios ya ili wasimamie kazi zote kwa muda wa miaka miwili.

Mkurugenzi wa kampuni ya uwakala ya One Touch Solution ya mjini Dar es Salaam, Petter Mwendapole alisema I-View itasimamia mikataba yote ya kazi zote za msanii huyo na yeyote atakayetaka kufanya kazi na Diamond kwa sasa itabidi awasiliane kampuni hiyo.


"Diamond ameamua kufanya kazi zake kimataifa. Ameingia mkataba na I-View ambao watakuwa wakisimamia maonyesho, matangazo, nyimbo kwenye simu, nguo na kila kitu kinachohusiana na yeye kinapaswa kupitia kwao," alisema.


Mwendapole alisema pamoja na maonyesho, kampuni hiyo pia itawajibika katika muonekano mpya wa msanii huyo anayetamba ndani na nje ya Tanzania na kwamba kampuni ya uwakala ya One Touch Solutions ndiyo watakaokuwa wasemaji wa msanii huyo.


Diamond kwa upande wake alisema anataka kufungua ukurasa upya katika tasnia ya muziki nchini na anaamini utasaidia katika kumfanya aongeze nguvu zaidi katika kutunga na kutengeneza nyimbo bora.


“Hii yote ni kuhakikisha nafanya kazi zangu kwa ufanisi badala ya kujirundikia mambo mengi, kuna watu walikuwa wakinitafuta wanashindwa kunipata lakini sasa watakuwa wanafahamu ofisi ziko wapi na wanawasiliana na menejimenti, watu wa habari watakuwa na mtu wa kuwasiliana naye moja kwa moja hata kama sipatikani,” alisema.


Diamond anatarajia kutoa wimbo wake mpya ambao pia utarekodiwa na kampuni ya I-View. Tayari usaili umeshafanyika kwa ajili ya wale ambao wataonekana kwenye video ya wimbo huo.


I-View mbali na kazi kupiga picha, lakini pia inatengeneza matangazo mbalimbali ya TV, Radio, mabango, ubunifu wa kazi mbalimbali za sanaa.

No comments:

Post a Comment