Tuesday, October 2, 2012

SUMAYE APATA PIGO URAIS 2015

Frederick Sumaye
NDOTO za Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye za kuwania Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, zimeingia doa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara. Sumaye ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo la Hanang kwa kipindi kirefu hadi mwaka 2005, ameshindwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk Mary Nagu ambaye amegeuka kuwa mmoja wa hasimu wake wa kisiasa katika siku za karibuni, mbali ya kuwa na mahusiano mazuri kwa miaka mingi.

 Taarifa za Sumaye kushindwa zilianza kuvuja mapema hata kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo saa 10:00 alfajiri jana, kwani baadhi ya wapambe wake walilazimika kuondoka katika ukumbi uliokuwa ukifanyika uchaguzi huo. Msimamizi wa uchaguzi huo ulianza kufanyika juzi asuhubi, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo akitangaza matokeo hayo alisema Sumaye alipata kura 481 huku Dk Nagu akiibuka mshindi kwa kupata kura 648. 

Mgombea mwingine, aliyekuwa anawania nafasi hiyo, Leonce Marmo Bura alitangaza kujitoa mapema ili apate fursa ya kugombea nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambao alishinda. Dk Nagu tangu awali alionekana kuungwa mkono na wajumbe wengi wa mkutano huo hali ambayo ilimfanya wakati wa kujieleza asiulizwe maswali huku mwenzake Sumaye akibanwa kwa maswali mengi. 

Hata hivyo, uhodari za Sumaye, kujibu maswali hayo kwa kiasi fulani ulionekana kutaka kubadili hali ya upepo katika mkutano huo, lakini wakati wa kupiga kura nguvu ya Waziri Dk Nagu ilionekana kurejea upya. Mvutano kati ya Sumaye na Nagu ulianza kuonekana hivi karibuni baada ya kikao cha kamati ya siasa ya Wilaya kilichofanyika Septemba 2, mwaka huu kupitisha jina la Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo huku la Nagu likiondolewa kufuatia kudaiwa kuwa na majukumu mengi ya kikazi ikiwamo Ubunge na Uwaziri. Hata hivyo, Nagu alikata rufaa katika Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara ambayo ilirejesha jina lake. 

Kushindwa kwa Sumaye kupata nafasi hiyo kunaonyesha ni kikwazo kipya kwake kama ataamua kuwania Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa mara nyingine. Sumaye ambaye amekuwa Waziri Mkuu katika utawala wote wa Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa aliwania Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, akishindana na Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, Dk Abdallah Kigoda na Profesa Mark Mwandosya. 

Hata hivyo, pamoja na kwamba hajaweka wazi kuwa atagombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2015, lakini watu walio karibu na mwanasiasa huyo wamekuwa wakieleza kuwa anajiandaa kugombea tena nafasi hiyo. Juzi wakati akijieleza mbele ya wajumbe wa mkutano huo, Sumaye alionekana kushangazwa na hatua ya Dk Nagu kugombea nafasi hiyo, hali akijua kuwa yeye ni Waziri na hivyo kwa utaratibu ndani ya CCM ni mjumbe moja kwa moja wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
 Kwa upande wa Dk Nagu ambaye aliachiwa kugombea ubunge wa jimbo hilo na Sumaye mwaka 2005, katika siku za karibuni amekuwa akitamba kuwa ni Simba jike, alitumia dakika tatu za kujieleza kukanusha uvumi kuwa ametumwa na makundi mengine ndani ya CCM ili kumzuia Sumaye asiwe Mjumbe wa NEC ikiwa ni harakati za kugombea Urais mwaka 2015. 
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment