Friday, September 28, 2012

JOHN TERRY AFUNGIWA MECHI NNE...NI BAADA YA KUKUTWA NA HATIA YA VITENDO VYA UBAGUZI WA RANGI DHIDI YA ANTON FERDINAND WA QPRJohn Terry (kulia) na Anton Ferdinand (kushoto)
LONDON, England
Nahodha wa Chelsea, John Terry amefungiwa mechi nne na kutozwa faini ya paundi za England 220,000 (Sh. milioni 550) na Chama cha Soka cha England baada ya kukutwa na hatia ya kumfanyia vitendo vya ubaguzi wa rangi beki wa QPR, Anton Ferdinand.

Terry alisafishwa Julai kwa kuonekana hana hatia ya kumbagua Ferdinand na Mahakama ya Hakimu Mkazi  Westminster, lakini kamati ya nidhamu ya FA imetangaza kwamba beki huyo mwenye miaka 31 amekutwa na hatia ya kumfanyia vitendo vya ubaguzi Ferdinand kwa kuangalia mazingira ya tukio, na sio kumkuta na kosa pasi na shaka yoyote.

Tukio hilo lilitokea Loftus Road Oktoba 23, 2011, wakati Terry na Ferdinand walipokwaruzana wakati wa mechi yao ambayo QPR ilishinda 1-0 dhidi ya Chelsea.

Nyota huyo wa Chelsea alitangaza kustaafu kucheza mechi za kimataifa akiwa na timu ya taifa ya England muda mfupi kabla ya kusikilizwa kwa kesi yake na FA, akisema kwamba chama cha soka kimemfanya awe katika wakati mgumu kuitumikia timu hiyo baada ya kuamua kuendesha kesi dhidi yake.

Terry ana siku 14 za kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na FA, ambayo ilifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza ushahidi kwa siku nne kwenye Uwanja wa Wembley.

No comments:

Post a Comment