Monday, October 1, 2012

JOSE MOURINHO: JOHN TERRY HAJAWAHI KUWA MBAGUZI WA RANGI..WAULIZENI KINA DROGBA, ESSIEN..

LONDON, England
Kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho amejitosa kumtetea nahodha wa klabu hiyo John Terry, akisema kwamba beki huyo si mbaguzi.

Terry alipewa ahabu ya kufungiwa mechi nne na Chama cha Soka cha England (FA) Alhamisi baada ya kukutwa na hatia ya kumfanyia vitendo vya ubaguzi beki wa Queens Park Rangers, Anton Ferdinand katika mechi yao ya Ligi Kuu ya England msimu uliopita.

Terry ambaye ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya England, aliyetangaza kustaafu soka la kimataifa Jumapili iliyopita, bado hajaamua kama akate rufaa ama la.

"Chelsea ilikuwa na kikosi ambacho ndani yake kulikuwa na wachezaji 12," kocha wa Real Madrid, Mourinho, aliyeiongoza Chelsea kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya England, amesema katika mahojiano yake na CNN juzi.

"Kilikuwa ni kikosi safi sana na siku zote Terry alikuwa na mahusiano mazuri na kila mmoja. Tafadhali msimwite mbaguzi, kwa sababu ninajua hiki ninachokisema.

"(Wachezaji wa zamani wa Chelsea) Didier Drogba atasema, Geremi atasema, Claude Makelele atasema, wote hawa watasema yeye si mbaguzi."

Terry alisafishwa na tuhuma za ubaguzi mahakamini mwezi Julai lakini uamuzi wa FA kuendelea na kesi kivyao dhidi yake ulifuatiwa na uamuzi wa beki huyo wa kati kutangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya nchi yake.

Wakati akimuunga mkono nahodha wake wa zamani, kocha wa Ureno, Jose Mourinho hakutaka kupinga kwamba Terry hakumtusi kibaguzi Ferdinand.

"Inaweza kutokea wakati wa mechi yoyote ya soka - kwa sababu wakati mwingine huwa ni zaidi ya mchezo - wakati mwingine unajibu kwa namna ambayo haiendani na tabia yako," Mourinho amesema.

Terry alicheza wakati Chelsea ambao ni vinara kwenye msimamo wa ligi wakishinda ugenini 2-1 dhidi ya Arsenal jana kwa sababu adhabu yake ya kufungiwa hataanza kuitumikia hadi hapo atakapoamua kama atakata rufaa ama la.

No comments:

Post a Comment