MECHI YA SIMBA NA YANGA YAINGIZA TSHS 390...KLABU ZAAMBULIA MIL 93
MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom baina ya
watani wa jadi Yanga na Simba iliyochezwa jana (Oktoba 3 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1
imeingiza Sh. 390,568,000, lakini makato makubwa kupitiliza katika
uwanja huo yameendelea kutozinufaisha klabu.
Katika mgawo, Yanga na Simba kila moja
zimepata Sh.milioni 93 ambazo jumla yake inakuwa ni Sh. milioni 186
wakati makato ni mengi zaidi kiasi ambacho klabu hizo mbili zinapata.
Jumla ya makato ni Sh. milioni 203.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, watazamaji 50,455 walikata
tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa 1 usiku kwa
viingilio vya Sh. 5,000, Sh. 7,000, Sh. 10,000, Sh. 15,000, Sh. 20,000
na Sh. 30,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa Sh. 93,345,549.15 wakati
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni Sh. 59,578,169.49.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 240,000,
kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 591,000, mwamuzi wa akiba
(reserve referee) sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na
Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
Umeme sh.
750,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa
mechi sh. 5,860,000 wakati tiketi ni sh. 7,327,000. Gharama za mchezo
sh. 31,115,183.05, uwanja sh. 31,115,183.05, Kamati ya Ligi sh.
31,115,183.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
18,669,109.83 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 12,446,073.22.
Wakati huo huo, mechi ya ligi hiyo kati ya
African Lyon na Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex na
kushuhudiwa na washabiki tisa kwa kiingilio cha sh. 3,000 imeingiza sh.
27,000.
Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa VAT sh. 4,118.6 wakati kila
timu ilipata sh. 6,864.3. Uwanja sh. 2,288.1, gharama za mchezo sh.
2,288.1, Kamati ya Ligi sh. 2,288.1, FDF sh. 1,372.8 na DRFA sh. 915.2
Katika
mechi hiyo, kiungo Amri Kiemba aliifungia Simba goli lao katika dakika 4
kufuatia krosi ya Mwinyi Kazimoto kabla ya Yanga kusawazisha kupitia
kwa straika Said Bahanunzi katika dakika ya 65 kwa penalti iliyotolewa
na Mathew Akrama baada ya
beki wa Simba, Paul Ngalema kushika mpira ndani ya 18 wakati akijaribu kuokoa mpira wa kona kwa kichwa.